Saturday, 3 March 2012

IMANI POTOFU KUHUSU AFYA YA KINYWA NA MENO


Na Dr. Augustine Mbehoma Rukoma
Asante kwa mtandao kwani habari zinasambaa haraka kama mwanga. Hata hivyo, uvumi, imani potofu vinasambaa kwa kasi ile ile pia. Hii inahusisha imani potofu kuhusu afya ya kinywa na meno. Kwa hiyo,
nafikiri ni bora kuchukua muda kidogo kuweka baadhi mambo sawa kuhusu afya ya kinywa na meno.
Baadhi ya imani potofu ni kama ifuatavyo:-

1.      POTOFU: Kupiga mswaki mara nyingi na kwa nguvu huzuia kuoza kwa meno
UKWELI: Si mara ngapi unapiga mswaki na nguvu gani inatumika, suala ni unapigaje mswaki. Kupiga mswaki mara nyingi na kwa maguvu kunaweza kupleleke kukwangua sehemu ngumu ya nje ya jino, kulifanya laini na hatimaye kuuma au hata kuvunjika. Kupiga mswaki mara mbili, taratibu na kwa njia sahii ndicho kinachosaidia meno kuwa na afya

2.      POTOFU: Huna haja ya kumuona tabibu wa meno kama hujaona au kuhisi una tatizo la meno.
UKWELI: kila mtu anatakiwa kumuona tabibu wa meno angalau mara mbili kwa mwaka bila kujari meno yake yanaonekana vizuri au imara kiasi gani. Si meno yote yanayoonekana mazuri na imara ni mazima, mengine yanaweza kuwa yameoza katika maeneo usiyoweza ona kama chini ya fizi na kwenye mizizi, si hivyo tu hata uoto mpya (neoplasm) uweza kugundulika mapema kabla ya kufanya uaribifu mkubwa kama utachunguzwa na wataalamu. Kumbuka pia mangonjwa ya mifumo mingine kama ukimwi,
kisukari na mengine mengi hujidhihilisha mapema kinywani kabla mgonjwa hajapata dalili zingine.

3.      POTIFU: Husile kitu chochote unapokwenda kung’oa jino
UKWELI: Njaa inaweza kukufanya uzirahi katika zoezi la kungoa jino, hofu ikichanganyika na sukari kidogo mwilini husababisha ubongo kushindwa kufanya kazi sawa sawa. Imani hii potofu inahusishwa na
sindano ya ganzi, watu wengi wanafikiri kila ganzi inatakiwa mtu awe hakula kwa muda Fulani. Hii kwa matibabu ya meno sio kweli kwani ganzi utolewa kwenye eneo husika tu (local anaesthesia) hivyo haiathili mwili mzima.

4.      POTOFU: Husitoe jino au kufanya matibabu ya mzizi wa jino kama una uvimbe hasa usaa
UKWELI: Kung’oa jino au matibabu ya mzizi wa jino yanasaidia kutoa nafasi/njia kwa usaa kutoka na hivyo kupona haraka pengine bila hata kuhitaji dawa (antibiotics). Yaweza kuwa kweli pale tu kama mgonjwa atukuwa na homa au hawezi fungua kinywa ambapo itabidi udhibiti homa kwanza, na kama ni
kushindwa kufungua kinywa yabidi kuacha na kutibu kinacho mfanya ashindwe kufungua kinywa kwanza.

5.      POTOFU: Mama mjamzito hastahiri kutoa jino mpaka atakapo jifungua
UKWELI: Kumuacha mama mjamzito na maumivu pamoja na ugonjwa kwaweza kufanya ugonjwa kusambaa na kuingia kwenye ubongo hata kupelekea kifo cha mama na mimba yake. Pia maumivu makali yaweza kusababisha mimba kutoka.

6.      POTOFU: Njia ya uhakika ya kutibu jino ni kuling’oa
UKWELI: Ziko njia nyingi na za uhakika za kutibu jino bila kungoa. Kung’oa jino kama tiba ni pale tu ambapo jino hilo haliwezi tibika kwa njia yeyote na kukaa kwake kwa weza leta madhara zaidi. Kutoa jino huleta madhara mengine na meno bandia pamoja na kwamba hayawezi kurejesha kazi za meno yaliyotoka kwa kiwango halisi, lakini pia utunzaji wake ni mgumu na gharama pia. Hata hivyo kama umelazimika kupoteza meno basi meno bandia ndilo chaguo pekee.

7.      POTOFU: Kuweka dawa ya kutuliza maumivu kama aspirini kwenye tobo kunasaidia kutoa maumivu.
UKWELI: Kama ilivyo kwa magonjwa mengine, kutuliza maumivu wakati kisababishi cha maumivu hakijashugulikiwa ni kulikuza tatizo kwa gharama. Mbali na hivyo dawa kama aspirini uunguza fizi zilizozunguka jino ulimoiweka, pia ulilainisha? (weaken) na kufanya uotaji wake uwe
mgumu kwani uvunjika vunjika ovyo ovyo

8.      POTOFU: Kutoa jino husababisha kifo
UKWELI: kuendelea kukaa na jino lililooza na halifai kuzibwa hufanya ugonjwa kusambaa na kusababisha kifo. Unaonekana kama ukweli pale tu mgonjwa anakuja hospitalini kutoa jino
9.      POTOFU: Meno mazuri urithishwa (inherited)
UKWELI: Eti kwa vile tu mama au baba ana meno mazuri na mazima na wewe utakuwa hivyo au kinyume chake. Uridhi unachangia kiasi kidogo sana, utunzaji wa meno vizuri na kukutana na tabibu wa meno mara kwara ndio mambo muhimu ya kuweka meno na kinywa chako sawa.

10.     POTOFU: Hakuna haja ya kuangaika na meno ya utotoni kwani yatatoka baada ya muda wake kufika
UKWELI: meno ya utotoni yasipotunzwa vizuri yanaweza kusababisha kutoka/ kutolewa kabla ya muda wake na kupeleke meno ya ukubwani kuota kwa mpangilio usiopendeza, lakini pia katika kipindi cha mchanganyiko wa meno ya ukubwani na utotoni, meno ya utotoni yaliyooza yaweza ambukiza ya ukubwani.

11.     POTOFU: Maumivu ya meno yatajiishia yenyewe baada ya muda.
UKWELI: Kama jino limeoza haliwezi pona kwa namna yoyote mpaka lipate tiba hata kama haliumi. Ukiendelea kulidharau ugonjwa uweza kusambaa mpaka maeneo mengine kama ubongo, kifuani na hatimaye kusababisha kifo.
Angalizo: Ni asilimia tano tu kati ya wagonjwa ambao tatizo la jino
limesambaa hadi kwenye ubongo uweza kupona.

Tafakari chukua hatua 2012